Na: ERNEST BONIFACE MAKULILO
CALIFORNIA, USA
Kumekuwepo na sintofahamu kwa watu wengi katika dhana kuu mbili, Udahili
na Udhamini. Sintofahamu hii imepelekea watu kuanza kuwa na imani
potofu kuwa upatikanaji wa udhamini ughaibuni ni suala la bahati. Katika
makala hii ninaelezea nini maana ya udahili na udhamini, na kipi
kinaanza na kipi kinafuata. Pia nitaelezea uchaguzi wa mchapuo wa kusoma
ikihusishwa na udhamini uliopo katika chuo husika.
Udahili ni ile hatua ya mtu kufanya maombi katika chuo husika na kutaka
kusoma shahada itolewayo katika chuo hicho. Hatua hii haina maana kwamba
mara upatapo udahili huo basi unapewa ufadhili wa kusoma katika chuo
husika. Hili limekuwa tatizo kubwa kwa watu wengi, wao wanaomba udahili
bila kuangalia kwamba mchapuo huo walioomba katika chuo hicho watapata
ufadhili au la. Maswali ya kujiuliza ni kipi unatakiwa kuangalia kwanza
katia ya udahili katika chuo ukipendacho na ufadhili unaopatikana? Kipi
cha kuzingatia kati ya uchaguzi wa mchapuo (degree program) na uwepo wa
udhamini?
Kwa ufupi ni kwamba unapokuwa na mpango wa kusoma ughaibuni na unatafuta
udhamini ili uweze kusoma huko, kitu cha kwanza ni kuangalia ni chuo
kipi wanatoa udhamini wa kozi mbalimbali. Unapotambua vyuo husika
ambavyo wanatoa udhamini kwa wanafunzi wa kimataifa, kifuatacho ni
kuangalia sasa ni michapuo ipi katika vyuo hivyo. Ukishapata kujua ni
vyuo vipi vinatoa udhamini na kwenye michapuo ipi hapo unaweza sasa amua
kuchagua usome mchapuo upi.
Tatizo la watu wengi ni kwamba wao wanaanza kuchagua mchapuo wa kusoma
bila kuangalia je chuo husika wana udhamini katika mtaala huo. Mfano
dhahiri ni huu hapa: Mimi nilisoma shahada yangu ya kwanza ya Sayansi ya
Siasa na Utawala wa Umma toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati
nataka kusoma Shahada yangu ya Uzamili (Masters) kabla sijaanza kusema
nataka kusoma mchapuo gani, kitu kwanza niliangalia ni vyuo vipi na nchi
zipi zinatoa udhamini wa elimu ya shahada ya uzamili kwa mtu ambaye ana
shahada ya Sayansi ya Siasa. Na baada ya kutambuo vyuo/nchi hizo,
nikaangalia ni michapuo ipi inapewa udhamini mkubwa hasa kwa wanafunzi
wa kimataifa, na kisha nikaanza kutafuta ni michapuo ipi inaendana name
na malengo yangu.
Mfano huo hapo ni kwamba usianze kusema mimi lazima nisome MA Conflict
Resolution bila kujua je, ni vyuo vingapi na nchi zipi zinatoa mchapuoa
huo. Na je, katika vyuo hivyo/nchi hizo ni vipi vinatoa udhamini kwa mtu
kusoma hapo. Athari za mtu kuanza na dhana ya kuchaguo mchapuo ni
kuanza kufanya maombi ya udahili bila ya kuzingatia uwepo wa ufadhili
kwa wanafunzi wa kimataifa ni mtu kupata udahili usio na udhamini, yaani
ukitakiwa kujilipia mwenyewe ili hali wewe haina fedha za kujisomesha.
Na pia usitegemee kusema ngoja niombe udahili na nikishapa basi nitaanza
kutafuta wafadhili sehemu mbalimbali kunisaidia kulipia masomo yangu.
Tarehe ya mwisho ya utumaji maombi (Deadline) ni muhimu sana
kuzingatiwa. Kitu cha kwanza muombaji lazima ajue ni kwamba kwa
wanafunzi wa kimataifa na wanakwenda kusoma ughaibuni kwa udhamini
wanatakiwa kuanza masomo yao Muhula wa Majira ya Vuli (Fall/Autumn
Semester) ambao ni kuanzia mwezi wa nane, Agosti. Hivyo basi ni vyema
kutambua ni lini mtu utume maombi yako na ni lini utajua kama umepata
udahili na ufadhili.
Muda wa utumaji wa maombi huanzia mwezi wa nane, Agosti hadi mwishoni
mwa Desemba. Na kuna baadhi ya vyuo wao maombi huendelea hadi mwanzoni
mwa Februari kila mwaka. Mfano kama umetuma maombi yako Agosti 2011 au
Desemba 2011 basi utaanza masomo Agosti 2012. Na endapo ukiomba na
kukosa basi mwombaji huyo atatakiwa kuomba tena Agosti-Desemba 2012 na
kusubiria kuanza kusoma Agosti 2013.
Kama kweli una nia ya kusoma ughaibuni kwa kupitia ufadhili, basi huna
budi kujua kalenda hiyo ya uombaji. Na kama nilivyoelezea hapo juu, ni
vyema mwombaji kuhakikisha unatuma maombi mengi sana kwa kima chini
maombi 15 ili kuweza kujihakikishia angalau kupata udahili na udhamini
katika chuo kimoja. Ushindani ni mkubwa mno hivyo kama ukizembea na
kufanya maombi machache unakuwa unaongeza muda wako wa lini upate
udhamini, ila kama ukiomba vyuo vingi basi unajiongezea uwezekano wa
kupata udhamini haraka.
Baada ya kuangalia mambo muhimu kabla ya kuanza kufanya maombi yako
katika makala hii na zilizopita, kuanzia makala zijazo tutaanza
uchambuzi wa hatua moja baada ya nyingine ya kufanya maombi ya
ushindani. Na pia uchambuzi utaelezea baadhi ya udhamini kama vile Quota
Scheme, Fulbright, Rotary Ambassadorial, Nuffic nk.
Unaweza kujiunga na Jukwaa langu la Udhamini/Ufadhili wa elimu (MAKULILO SCHOLARSHIP FORUM)
www.scholarshipnetwork.ning.com na ukijiunga hapo utaweza kuwa unapokea fursa za ufadhili ughaibuni moja kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kwa maswali au maoni, niandikie
Makulilo@makulilofoundation.org
Ernest_makulilo@yahoo.com
MAKULILO, JR.