Na: ERNEST BONIFACE MAKULILO
CALIFORNIA, USA
Kumekuwepo na sintofahamu kwa watu wengi katika dhana kuu mbili, Udahili na Udhamini. Sintofahamu hii imepelekea watu kuanza kuwa na imani potofu kuwa upatikanaji wa udhamini ughaibuni ni suala la bahati. Katika makala hii ninaelezea nini maana ya udahili na udhamini, na kipi kinaanza na kipi kinafuata. Pia nitaelezea uchaguzi wa mchapuo wa kusoma ikihusishwa na udhamini uliopo katika chuo husika.
Udahili ni ile hatua ya mtu kufanya maombi katika chuo husika na kutaka kusoma shahada itolewayo katika chuo hicho. Hatua hii haina maana kwamba mara upatapo udahili huo basi unapewa ufadhili wa kusoma katika chuo husika. Hili limekuwa tatizo kubwa kwa watu wengi, wao wanaomba udahili bila kuangalia kwamba mchapuo huo walioomba katika chuo hicho watapata ufadhili au la. Maswali ya kujiuliza ni kipi unatakiwa kuangalia kwanza katia ya udahili katika chuo ukipendacho na ufadhili unaopatikana? Kipi cha kuzingatia kati ya uchaguzi wa mchapuo (degree program) na uwepo wa udhamini?
Kwa ufupi ni kwamba unapokuwa na mpango wa kusoma ughaibuni na unatafuta udhamini ili uweze kusoma huko, kitu cha kwanza ni kuangalia ni chuo kipi wanatoa udhamini wa kozi mbalimbali. Unapotambua vyuo husika ambavyo wanatoa udhamini kwa wanafunzi wa kimataifa, kifuatacho ni kuangalia sasa ni michapuo ipi katika vyuo hivyo. Ukishapata kujua ni vyuo vipi vinatoa udhamini na kwenye michapuo ipi hapo unaweza sasa amua kuchagua usome mchapuo upi.
Tatizo la watu wengi ni kwamba wao wanaanza kuchagua mchapuo wa kusoma bila kuangalia je chuo husika wana udhamini katika mtaala huo. Mfano dhahiri ni huu hapa: Mimi nilisoma shahada yangu ya kwanza ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wakati nataka kusoma Shahada yangu ya Uzamili (Masters) kabla sijaanza kusema nataka kusoma mchapuo gani, kitu kwanza niliangalia ni vyuo vipi na nchi zipi zinatoa udhamini wa elimu ya shahada ya uzamili kwa mtu ambaye ana shahada ya Sayansi ya Siasa. Na baada ya kutambuo vyuo/nchi hizo, nikaangalia ni michapuo ipi inapewa udhamini mkubwa hasa kwa wanafunzi wa kimataifa, na kisha nikaanza kutafuta ni michapuo ipi inaendana name na malengo yangu.
Mfano huo hapo ni kwamba usianze kusema mimi lazima nisome MA Conflict Resolution bila kujua je, ni vyuo vingapi na nchi zipi zinatoa mchapuoa huo. Na je, katika vyuo hivyo/nchi hizo ni vipi vinatoa udhamini kwa mtu kusoma hapo. Athari za mtu kuanza na dhana ya kuchaguo mchapuo ni kuanza kufanya maombi ya udahili bila ya kuzingatia uwepo wa ufadhili kwa wanafunzi wa kimataifa ni mtu kupata udahili usio na udhamini, yaani ukitakiwa kujilipia mwenyewe ili hali wewe haina fedha za kujisomesha. Na pia usitegemee kusema ngoja niombe udahili na nikishapa basi nitaanza kutafuta wafadhili sehemu mbalimbali kunisaidia kulipia masomo yangu.
Tarehe ya mwisho ya utumaji maombi (Deadline) ni muhimu sana kuzingatiwa. Kitu cha kwanza muombaji lazima ajue ni kwamba kwa wanafunzi wa kimataifa na wanakwenda kusoma ughaibuni kwa udhamini wanatakiwa kuanza masomo yao Muhula wa Majira ya Vuli (Fall/Autumn Semester) ambao ni kuanzia mwezi wa nane, Agosti. Hivyo basi ni vyema kutambua ni lini mtu utume maombi yako na ni lini utajua kama umepata udahili na ufadhili.
Muda wa utumaji wa maombi huanzia mwezi wa nane, Agosti hadi mwishoni mwa Desemba. Na kuna baadhi ya vyuo wao maombi huendelea hadi mwanzoni mwa Februari kila mwaka. Mfano kama umetuma maombi yako Agosti 2011 au Desemba 2011 basi utaanza masomo Agosti 2012. Na endapo ukiomba na kukosa basi mwombaji huyo atatakiwa kuomba tena Agosti-Desemba 2012 na kusubiria kuanza kusoma Agosti 2013.
Kama kweli una nia ya kusoma ughaibuni kwa kupitia ufadhili, basi huna budi kujua kalenda hiyo ya uombaji. Na kama nilivyoelezea hapo juu, ni vyema mwombaji kuhakikisha unatuma maombi mengi sana kwa kima chini maombi 15 ili kuweza kujihakikishia angalau kupata udahili na udhamini katika chuo kimoja. Ushindani ni mkubwa mno hivyo kama ukizembea na kufanya maombi machache unakuwa unaongeza muda wako wa lini upate udhamini, ila kama ukiomba vyuo vingi basi unajiongezea uwezekano wa kupata udhamini haraka.
Baada ya kuangalia mambo muhimu kabla ya kuanza kufanya maombi yako katika makala hii na zilizopita, kuanzia makala zijazo tutaanza uchambuzi wa hatua moja baada ya nyingine ya kufanya maombi ya ushindani. Na pia uchambuzi utaelezea baadhi ya udhamini kama vile Quota Scheme, Fulbright, Rotary Ambassadorial, Nuffic nk.
Unaweza kujiunga na Jukwaa langu la Udhamini/Ufadhili wa elimu (MAKULILO SCHOLARSHIP FORUM) www.scholarshipnetwork.ning.com na ukijiunga hapo utaweza kuwa unapokea fursa za ufadhili ughaibuni moja kwa moja kwenye barua pepe yako.
Kwa maswali au maoni, niandikie
Makulilo@makulilofoundation.org
Ernest_makulilo@yahoo.com
MAKULILO, JR.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni